Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto kunyonyeshwa saa ya kwanza tu baada ya kuzaliwa ni muhimu kwa uhai wake

Mtoto kunyonyeshwa saa ya kwanza tu baada ya kuzaliwa ni muhimu kwa uhai wake

Pakua

Kuelekea kuanza kwa wiki ya unyonyeshaji duniani tarehe mosi mwezi ujao, shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema watoto 3 kati ya 5 wanakosa fursa ya kunyonya maziwa ya mama zao punde tu wanapozaliwa na hivyo kuwaweka hatarini kupata magonjwa na pia kufariki dunia.

Kilio cha mtoto mchanga hicho, kikiashiria heri baada ya mama yake kujifungua! Ni kwenye moja ya vituo vya afya nchini Nigeria. Wakunga wamempokea mtoto huyu taratibu za vipimo zinaendelea.

 

Kwa mtoto huyu na wengine wengi, mustakhbali wa uhai wao uko mashakani kwa kuwa wanakosa maziwa ya mama ndani ya kipindi cha saa moja tangu kuzaliwa.

 

Kupitia ripoti  yake iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi, WHO inasema watoto milioni 78 ulimwenguni kote hawapati maziwa ya mama punde wanapozaliwa.

 

Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni watoto kupatiwa vinywaji vingine kando mwa maziwa ya mama pamoja na ongezeko la uzazi kwa upasuaji.

 

Maaike Arts ni mtaalamu wa lishe kutoka shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na anaelezea athari za mtoto kukosa maziwa ya mama punde tu akizaliwa akisema kuwa “Inasaidia kuanza kunyonyesha kwa usahihi, inazuia mtoto kufariki dunia miezi ya mwanzo ya uhai na pia inawakinga dhidi ya magonjwa.”

Misri imetolewa mfano ambako asilimia 19 tu ya watoto wanaozaliwa kwa njia ya upasuaji ndio wanapata fursa ya kunyonya maziwa ikilinganishwa na asilimia 39 ya watoto wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.

 

Huko jamhuri ya Dominika, kiwango cha wanaonyonyeshwa maziwa ya mama baada ya kuzaliwa kwa operesheni ni asilimia 40 ikilinganishwa na asilimia 61 ya wale wanaozaliwa kwa njia ya kawaida.

 

Hata hivyo ripoti inaweka bayana kuwa hata kujifungua kwa usaidizi wa mkunga mbobezi au kwenye kituo cha afya hakuongezi fursa ya mtoto kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, jambo linalothibitisha kuwa fursa hiyo sasa inakosekana kwa kila mtoto mchanga anayezaliwa.

 

 


 

Audio Credit
Siraj Kalyango
Audio Duration
2'16"
Photo Credit
unyonyeshaji