Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukarimu wa Bangladesh umeleta nuru kwa warohingya

Ukarimu wa Bangladesh umeleta nuru kwa warohingya

Pakua

Akiwa mjini Dhaka, nchini  Bangladesh hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mshikamano na wananchi wa Bangladesh pamoja na serikali yao ni muhimu kutokana na ukarimu wao kwa maelfu ya wakimbizi wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar waliosaka hifadhi nchini humo.
Bwana Guterres amesema hayo wakati akizungumza mjini Dhaka, kwenye tukio ambalo kwamo Bangladesh ilielezea mkakati wake wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.
Katibu Mkuu amesema katika zama za sasa ambazo mipaka mingi inafungwa ili kuzuia watu kuingia, Bangladesh na wananchi wake wamefungua milango yao na kuruhusu warohingya wanaokimbia vitendo vya ubakaji na mateso nchini mwao, waingie na waishi pamoja.
Pamoja na kuonyesha  mshikamano na nchi hiyo, Katibu Mkuu ameipongeza pia kwa kujumuisha malengo ya maendeleo endelevu kwenye mikakati ya nchi, akisema ndio njia mujarabu ya kuifanikisha. 
Hata hivyo amesema, “ni lazima jumuiya ya kimataifa isaidie katika kufanikisha mkakati wenu huu ili kuepusha vikwazo vya maendeleo kama vile usafirishaji haramu wa fedha. Ukiangalia bara kama la Afrika, fedha nyingi zinatoroshwa nje ya bara hilo na ambazo ni kiwango kikubwa kuliko hata kiwango chote cha misaada ya maendeleo ambayo bara hilo linapokea.”
Suala lingine ambalo amesema ni lazima lizingatiwe ili kufanikisha SDGs ni ujumuishaji wa wanawake na vijana akisema kuwa “vijana ni nguvu kazi ambayo ikitumiwa vyema italeta mabadiliko na ikipuuzwa italeta madhara kwani hushawishiwa na vikundi viovu.”
Na kuhusu wanawake amesema katika dunia ya leo ambayo idadi ya wanawake ni kubwa, ni lazima kuhakikisha uwakilishi wa nusu kwa nusu, akipongeza Bangladesh kwa kuwa na Waziri mkuu mwanamke. 
Bwana Guterres amesema kuwa na uwakilishi wa nusu kwa nusu katika ngazi zote za uongozi ni muhimu kwa kuwa..
(Sauti ya Antonio Guterres)
“Mnakuwa na ufanisi katika kushughulikia changamoto za usalama, changamoto za mizozo, changamoto za umaskini, changamoto za ukosefu wa usawa ambazo kwa ushiriki wa wanawake itatusaidia sana.”
Katibu Mkuu katika ziara hiyo anaambatana na Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, Kamishna Mkuu wa wakimbizi kwenye Umoja wa Mataifa Filippo Grand na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la idadi ya watu la umoja huo Nathalie Kanem.
Leo walitembelea shule moja mjini Dhaka ambako walielezewa na mmoja wa wanafunzi mwenye umri wa miaka 14 ni kwa jinsi gani wanafundishwa masuala ya afya ya uzazi.
Mapema Katibu Mkuu akiambatana na Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim walikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina ambapo pamoja na kumshukuru kwa ukarimu wao kwa warohingya walimweleza kuwa hatua za kushughulikia janga hilo la warohingya si wajibu wa Bangladesh pekee bali ni la dunia nzima.
Kesho Jumatatu Bwana Guterres na Bwana Jim wataelekea eneo la Cox’s Bazar ambako ndiko kimbilio la wakimbizi warohingya. Lengo la ziara hiyo itakayohusisha pia kuzungumza na wakimbizi hao na wenyeji wanaowahifadhi, ni kuonyesha mshikamano nao na kushukuru wenyeji hao kwa kitendo hicho cha upendo.
Idadi kubwa ya warohingya walianza kumiminika Cox’s Bazar kutoka Myanmar mwezi Agosti mwaka jana wakikimbia mateso, ukatili wa kingono na udhalilishwaji.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
UNICEF/Brian Sokol