Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa angalau wakimbizi warohingya walioko Cox's Bazar wanaweza kulala usingizi

Sasa angalau wakimbizi warohingya walioko Cox's Bazar wanaweza kulala usingizi

Pakua

Hatimaye eneo jipya la makazi kwa wakimbizi warohingya walioko Bangladesh limekamilika na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limefanikiwa kuwahamishia eneo hilo baada ya siku kadhaa za maandalizi ili kuwaepusha na mafuriko na maporomoko ya udongo yatokanayo na mvua za pepo za monsuni.

Huyu ni Aziz Fatima, mmoja wa wakimbizi warohingya kutoka Myanmar, ambaye sasa amenufaika na makazi mapya yaliyojengwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikina na wakimbizi wenyewe.

Anasema anapenda makazi yake mapya kwa kuwa hayapo tena kwenye mteremko, na zaidi ya yote nyumba ni thabiti na tayari imejengwa.

Makazi haya mapya yamejengwa kwenye eneo la Kutupalong, lililopo wilaya ya Cox Bazar nchini Bangladesh.

Nyumba hizi zimejengwa kwa kutumia mabanzi yaliyokatwa vipandevipande na kuunganishwa huku makaratasi ya nailoni yakifunika kama paa na kuta.

Kazi hii imefanywa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo UNHCR, lile la wahamiaji, IOM na la mpango wa chakula, WFP kwa kushirikiana na wakimbizi wenyewe waliofanya msaragambo, iwe kubeba mabanzi ya mianzi, iwe kubeba mchanga.

Kati ya wakimbizi 15,000 waliohamishiwa kwenye eneo hili jipya, baadhi yao walikuwa hawana makazi na wengine walikuwepo kwenye makazi ambayo yangaliporomoshwa na maji ya mafuriko.

Fred Cussigh, ni mratibu mwandamizi wa UNHCR na anasema sasa wanaendelea kuimarisha baadhi ya huduma za kijamii lakini...

 “Baadhi ya wanafamilia tuliozungumza nao tangu kuhamia makazi haya wana furaha sana na wameridhika. Wameelezea kuridhika na makazi haya kwani bi bora kuliko ya awali. Wanahisi wako salama kuliko walipokuwepo awali.”

UNHCR inasema wakimbizi wengine 200,000 wako hatarini kukumbwa na maporomoko ya udongo na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Kwa mantiki hiyo inahitaji eneo zaidi la ardhi lililo tambarare ili kujenga makazi na kuwahamishia maeneo salama.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'11"
Photo Credit
UNHCR/Caroline Gluck