Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvetiva kuokoa wakimbizi wa Rohingya Cox’s Bazar

Mvetiva kuokoa wakimbizi wa Rohingya Cox’s Bazar

Pakua

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesambaza zaidi ya miche milioni 2 ya mmea aina ya mvetiva kwa ajili ya kudhibiti mmomonyoko wa udongo kwenye kambi za wakimbizi wa kabila la Rohingya waliosaka hifadhi huko Bangladesh. Taarifa zaidi na Patrick Newman.

Hatua hiyo ya kutumia mvetiva, mmea unaofanana na mchaichai,  inalenga kudhibiti mmomonyoko wa  udongo unaonyemelea kambi hizo wakati huu wa kuelekea msimu wa pepo za monsuni.

IOM inasema miche mingine milioni 2 itapelekwa eneo hilo kabla ya mwisho wa mwezi huu kwa kuwa mradi wa awali umeonyesha mafanikio makubwa, huku wananchi wenyewe wakihusika na umwagiliaji ili isikauke.

Mratibu wa IOM kwenye upandaji wa miche hiyo Megan Genat amesema uamuzi wa kupanda mivetiva unatokana na walichojifunza kutoka chuo kikuu cha uhandisi na teknolojia cha Bangladesh katika kutumia mmea huo kudhibiti mmomonyoko wa udongo.

“Tumetiwa moyo sana na jinsi warohingywa walivyoitikia wito wa kutunza mimea hiyo na wameelewa athari za mmomonyoko wa udongo katika makazi yao,”amesema Bi. Genat.

Gharama ya mvetiva n idola 1.50 kwa miche 200 ambapo mradi mzima huko Cox’s Bazar utahusisha kupandwa kwa mimea hiyo kwenye eneo sawa na viwanja 150 vya mpira wa miguu.

Bi. Genat akazungumzia pia miradi mingine inayotekelezwa na IOM kando ya hiyo ya upanzi wa mivetiva akisema ni pamoja na ile ya kuboresha mazingira ya makazi kabla ya mvua ziambatanazo na pepo za monsuni.

“Katika kambi zote tunajenga barabara na kusafisha njia, tunaboresha mifereji ya maji, tunajenga madaraja na kuandaa maeneo haya kabla ya mvua. Tunashirikiana na mashirika mengine na mamlaka za Bangladesh kusaidia mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na majanga miongoni mwa wakimbizi na wenyeji,” amesema afisa huyo wa IOM.

Ghasia nchini Myanmar zilianza mwezi Agosti mwaka jana ambapo hadi sasa warohingya wapatao 700,000 wamevuka mpaka na kuingia eneo al Cox’s Bazar nchini Bangladesh.

Wakimbizi wapya wanahaha kusaka maeneo ya kujenga makazi yao kwa ajili ya familia ambapo maeneo yaliyosafishwa ili kujenga makazi yako kwenye mteremko na hivyo kuwaweka hatarini kukumbwa na mmomonyoko wa udongo.

Audio Credit
Patrick Newman
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
IOM/Fiona MacGregor