Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katu hatukubali watoto milioni 250 wawe mbumbumbu

Katu hatukubali watoto milioni 250 wawe mbumbumbu

Pakua

Umoja wa Mataifa leo umepokea ombi lililotiwa saini na vijana milioni 1.5 duniani la kutaka uwekezaji zaidi kwenye elimu.

Ombi hilo limewasilishwa leo jijini New York, Marekani na vijana watatu kwa Katibu Mkuu Antonio Guterres na mjumbe maalum wa elimu Gordon Brown.

Hatua ya vijana hao kutoka Kenya Sierra Leone na India inazingatia kuwa hivi sasa , watoto na barubaru milioni 264 hawako shuleni, fursa ya kupata elimu kuanzia ile ya chekechea hadi elimu ya juu ikizidi kuwa finyu.

Bwana Guterres amesema hali ni mbaya zaidi kwa watoto wa kike na wasichana ambao wao wanalazimika kusalia nyumbani kufanya kazi za kuteka maji na kulea familia ilhali kaka zao wanakwenda shule.

Amesema huko ni kuwakosesha haki yao ikiwemo ya kuendeleza vipaji vyao na kustawi ili hatimaye waweze kuchangia katika maendeleo yao na jamii zao.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Ndoto yetu ya mustakhbali endelevu inategemea kusaidia watoto wote wapate haki yao ya elimu. Hii inaamanisha mambo matatu; waanze mapema, kupatia kipaumbele walio pembezoni na kuchagiza usawa. Katika dunia yetu inayobadilika kwa kasi kubwa hatuwezi kukubali watoto milioni 250 washindwe kupata stadi za msingi.”

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema…

“Ndio maana mapendekezo haya ya chombo cha kimataifa cha uwekezaji kwenye elimu yanaweza kuwa muhimu. Hebu na tufanya yasiyowezekana yawezekane.”

Tukio hilo lilishuhudiwa pia na rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye ni kamishna wa jopo la watu mashuhuri la Umoja wa Mataifa kuhusu elimu.

Punde baada ya uzinduzi, jopo hilo lilizungumza na waandishi wa habari ambapo Kikwete aliulizwa ni kwa jinsi gani chombo hicho kilichozinduliwa kitaweza kusaidia Tanzania.

(Sauti ya Jakaya Kikwete)

Tatizo limekuwa ni kiwango, iwe ni cha walimu au vifaa vya kama vile vitabu na vifaa vingine . Serikali imeongeza bajeti ya elimu, imekuwa ni kipaumbele kwa zaidi ya asilimia 20. Lakini hiyo pekee haikutosheleza ndio maana serikali inahitaji msaada wa jamii ya kimataifa na ndio maana tunaona hatua kama hii ya chombo cha kimataifa cha kuchangisha fedha kwa ajili ya elimu kitakuwa na faida kubwa kwa serikali ya Tanzania.”

 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'50"
Photo Credit
Picha: © David Tett Photography / GEM Report