Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya kanuni mpya za maudhui ya mtandao yazuiliwa kwa muda Mtwara

Matumizi ya kanuni mpya za maudhui ya mtandao yazuiliwa kwa muda Mtwara

Pakua

Nchini Tanzania hii leo Mahakama Kuu kanda ya Mtwara imezuia kwa muda kuanza kwa matumizi ya kanuni mpya za maudhui ya mtandao nchini humo.

Kanuni hizo ambazo zilitakiwa kuanza kutumika rasmi tarehe 5 mwezi huu, zinataka pamoja na mambo mengine wamiliki wa blogu au watu wanaochapisha habari mtandaoni wawe wamesajiliwa, usajili ambao unafanyika kwa gharama.

Nimezungumza na Deodatus Balile, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania, TEF, ambao ni mmoja wa wadau sita waliowasilisha ombi la sitisho hilo mahakamani ambapo nimeanza kwa kumuuliza jinsi walivyopokea uamuzi huo.

(Mahojiano na Deodatus Balile)

Taasisi nyingine zilizowasilisha ombi hilo ni Legal and Human Rights Center (LHRC), Tanzania Human Rights Defenders (THRD), Media Council of Tanzania (MCT), Jamii Media, na Tanzania Media Women Association (TAMWA).

Katika kesi yao ya msingi ya mapitio ya kanuni hizo itakayoanza kusikilizwa tarehe 10 mwezi huu, taasisi hizo zimewashtaki Waziri wa Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wadau hao pamoja na mambo mengine wamesema kanuni zinakiuka kanuni za usawa, na zinapingana na haki ya kujieleza na haki ya usiri.

 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'22"
Photo Credit
Mitandao ya kijamii imeibuka na faida na changamoto zake hasa iwapo mtumiaji anakuwa hatambui sheria za matumizi. (Picha: World Bank/Arne Hoel)