Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yachachamaa Sudan Kusini, mchakato wa amani mashakani

Mapigano yachachamaa Sudan Kusini, mchakato wa amani mashakani

Pakua

Mapigano mapya yameripotiwa kwenye majimbo ya Unity, Jonglei na Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini na kusababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao huku vitendo vya ukatili wa kingono vikiripotiwa. 

Umoja wa Mataifa unasema milio ya risasi imesikika karibu na kituo chake cha muda huko Leer ambako walinda amani kutoka Ghana wanafanya doria kulinda wakimbizi wa ndani wapya 600 waliosaka hifadhi kwenye eneo hilo.

Ujumbe wa umoja huo nchini Sudan Kusini, UNMISS unasema raia wasio na hatia wamejikuta katikati ya mapigano, wanawake, watoto na wazee wakihaha kujinusuru.

David Shearer ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini na pia mkuu wa  UNMISS.

(Sauti ya David Shearer)

“Wafanyakazi wetu walioko eneo hilo wameripoti matukio ya mauaji, ukatili wa kingono, nyumba zinateketezwa, majangili wanapora mifugo na uporaji hospitalini na shuleni.”

Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya David Shearer)

“Tunasihi pande hasimu ziweke silaha chini, ziweke maslahi ya wananchi mbele na zishirikiane kujenga amani ya kudumu. Na viongozi wa kisiasa lazima waonyeshe wako tayari  kulegeza misimamo ili kutatua mzozo huu ambao unaleta madhara makubwa kwa wananchi wao.”

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'15"
Photo Credit
Picha: UM/Tim McKulka