Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji safi kunusuru utoro wa wanafunzi Uganda

Maji safi kunusuru utoro wa wanafunzi Uganda

Pakua

Wanafunzi 56,000 kutoka shule 100 za eneo la Karamoja, kaskazini-mashariki mwa Uganda sasa hawatokuwa na hofu tena ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama kufuatia makubaliano ya Umoja wa Mataifa na Korea Kusini. 

Makubaliano hayo yanahusisha mradi wa miaka mitano ya kujenga miradi ya maji safi na salama na huduma za kujisafi katika shule zilizoko wilaya zote 10 za Karamoja.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ambalo ndilo limetia saini makubaliano hayo na Korea Kusini limesema kupitia mradi huo watajenga vyoo, mitambo ya nishati ya jua pamoja na kuweka maji safi na salama kwa ajili ya kunywa na kujisafi ikiwemo kunawa mikono. Wanafunzi wa kike pia watapata elimu kuhusu hedhi salama.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Uganda Doreen Mulenga, amesema mradi utasaidia wanafunzi kuepuka utoro, magonjwa ya kuambukiza yatapungua na watoto watakuwa na fursa ya kujifunza kwa kina zaidi na hivyo kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu.

Mathalani amesema maji ya kunywa yatapatikana ndani ya umbali wa mita 500 shuleni badala ya wanafunzi kulazimika kutembea kwa nusu saa kusaka maji hayo kama wafanyavyo hivi sasa.

Mradi huo unagharimu dola milioni 10 ambapo Korea Kusini inachangia dola milioni 8 na UNICEF dola milioni  2.

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'28"
Photo Credit
Picha:Unicef/Zimbabwe/2016/NYAMANHINDI