Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chai na kunde ndio mlo wetu, tufanyeje?

Chai na kunde ndio mlo wetu, tufanyeje?

Pakua

Nchini Lebanon, wakimbizi wa Syria wanahaha kila uchao kuweza kukimu maisha yao ambapo hali ni ngumu zaidi kwa makundi yasiyojiweza ikiwemo wazee.

 

Huyu ni Shaalan Qaddour, mkimbizi wa Syria aliyeko hapa  Bhannine, nchini Lebanon,  ambapo mapigano nchini mwake yamemlazimu asake hifadhi ugenini yeye na familia yake akiwemo mkewe.

 

Shaalan mwenye umri wa miaka 90 anasema maisha ni magumu kwani analazimika kukopa fedha ili anunue dawa za kumtibu mkewe auguaye kisukari. Kwa mantiki hiyo wanalazimika kula supu kwa kunde.

 

(Sauti ya Shaalan Qaddour)

 

“Wakati mwingine tunatengeneza chai na kutoweza kwenye mkate. Tunakunywa chai tu na kumshukuru Mungu. Tufanyeje ?”


Idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria kama ilivyo kwa Shaalan, wanaishi kwenye umaskini. Miongoni mwao ni Sobhiya Homeid mkimbizi kutoka Homs nchini Syria. Yeye ni mjane mwenye watoto watano na kwa siku wanajikimu kwa chini ya dola tatu.

 

Sobhiya anasema wanapata msaada lakini bado haitoshi kwani fedha za mafuta wananunulia chakula na dawa


(Sauti ya Sobhiya Homeid)

 

 “Kama uonavyo, tunatumia kila kitu tunachopatiwa na bado haitoshelezi kwa sababu kila kitu ni aghali na mimi ni mgonjwa.”

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema ingawa watu wanapatiwa msaada bado hautoshelezi kwa kuwa gharama ya maisha ni ya juu.

 

Mireille Girard ni Mkuu wa UNHCR Lebanon.


(Sauti ya Mireille Girard)

 

 “Kwa sasa hali ya kuwa hatarini kwa wakimbizi hawa inaongezeka na sisi tunahaha kuhakikisha tunaendeleza kiwango cha usaidizi kama ilivyokuwa mwaka jana.”

 


UNHCR inasaidia familia 33,000 ambapo utafiti unaonyesha kuwa kiwango kikubwa cha fedha wanazopatiwa hutumika kulipia gharama ya pango, chakula na mafuta.

Shirika hilo limesema litahitaji dola bilioni 5.6 kwa mwaka huu ili kusaidia wakimbizi wa Syria waliotapakaa mashariki ya kati, na hadi sasani asilimia 27 tu ndio imepatikana.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'14"
Photo Credit
Mama mkimbizi kutoka Syria aliyekimbilia Lebanon.(Picha:UNHCR/A.McConnell)