Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani si bidhaa unatengeneza na kuuza

Amani si bidhaa unatengeneza na kuuza

Pakua

Hoja za nini kifanyike ili kuepusha mizozo na badala yake kuweka mazingira ya ujenzi wa amani endelevu zimewasilishwa hii leo kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na Baraza Kuu la umoja huo.

 

Viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo marais, wafalme, mawaziri wakuu na viongozi waandamizi wa nchi wanachama wametoa mitazam yao wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unasema kila kona mizozo inachipua na kule ambako ilishaanza inaota mizizi.

 

Mathalani Waziri wa Mambo ya Nje wa Norywa, Ine Eriksen Sÿreide amesema mwenendo na aina ya mizozo hivi sasa imebadilika ikilinganishwa na wakati Umoja wa Mataifa uliopoanzishwa miaka 72 iliyopita.

 

Kwa mantiki hiyo ametaka mbinu mpya na ushirikiano hasa katika ujenzi wa amani hususan katika kuzuia mizozo badala ya kuishughulikia.

 

Ushirikiano huo na ubia ni miongoni mwa mambo aliyotaja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hotuba yake akisema..

 

(Sauti ya Antonio Guterres)

 

“Kuwa na amani endelevu kutafanikiwa tu kupitia azma ya dhati, na mikakati ya kitaifa jumuishi na shirikishi ambayo inazingatia makundi yaliyo pembezoni zaidi, ikiwemo wanawake, vijana, makundi madogo na watu wenye ulemavu.”

 

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák amesema..

 

(Sauti ya Miroslav Lajčák)

 

“Kudumisha amani si zao la kuzalishwa na Umoja wa Mataifa. Si kitu tunachoweza kutengeneza hapa na kupeleka kwa mataifa na jamii. Tutafanikiwa tu iwapo tutakuwa na ubia.”

Mkutano huo wa siku mbili utamalizika kesho.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'35"
Photo Credit
Picha na UN/Staton Winter