Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi waendelea wa vifo vya watu 45 nchini Yemen

Uchunguzi waendelea wa vifo vya watu 45 nchini Yemen

Pakua

Umoja wa Mataifa unaendelea na uchunguzi kubaini utambulisho wa wahanga wa mashambulizi ya anga yaliyofanyika siku nne zilizopita nchini Yemen na kusababisha vifo vya watu 45. 

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa waliouawa ni pamoja na wanawake na watoto, huku mamia wengine wakiwa wamejeruhiwa.

Katika shambulio la kwanza la anga muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulishambulia basi la abiria karibu na Kijiji cha Al-Areish wilaya ya Mawza jimboni Taiz na kuua watu 21 wakiwemo watoto watano. 

Liz Throssell ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva, Uswisi.

(SAUTI YA LIZ THROSSELL)

“Watu walioshuhudia wanasema watu hao walikuwa wanarejea nyumbani kupitia barabara ndogo ya kijijini kombora la anga liliposambaratisha gari lao. Miili ya wahanga wa tukio hilo iliungua vibaya kiasi kwamba ni vigumu kuitambua.”

Shambulio la pili lilitokea Jumapili na kujeruhi watu wengi na la kusikitisha zaidi ni lile la kwenye sherehe ya harusi Jumatatu jimboni Haijah lililokatili maisha ya raia 19 na kujeruhi wengine 50. 

Ofisi ya haki za binadamu imeutaka muungano unaoongozwa na Saudia Arabia kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa mauaji yote hayo ya karibuni. 

 

Tangu kuanza kwa machafuko Yemen Machi 2015 raia zaidi ya 6,300 wameuawa na 9,900 wamejeruhiwa.

 

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'22"
Photo Credit
Miongoni mwa wahanga wa mashambulizi Yemen ni watoto. (Picha:UNICEF/UN013947/Shamsan) MAKTABA