Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpiga picha wa maandamano Misri ashinda tuzo ya UNESCO

Mpiga picha wa maandamano Misri ashinda tuzo ya UNESCO

Pakua

Mcheza kwao hutunzwa, na ndivyo ilivyokuwa kwa raia wa Misri Mahmoud Abu Zeid, ambaye ameshinda tuzo ya mwaka huu ya uhuru wa vyombo vya habari ya Guillermo Cano.

Abu Zeid al maarufu Shawkan, ameshinda tuzo hiyo inayotolewa na UNESCO ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni.

Shawkan amekuwa kizuizini tangu Agosti 14 mwaka 2013 ambapo alikamatwa wakati akipiga picha za  maandamano kwenye eneo la Rabaa Al-Adawiyya mjini Cairo nchini Misri.

Mwaka 2017 mwendesha mashtaka wa kesi dhid yake, aliomba Shawkan ahukumiwe adhabu ya kifo.

Hata hivyo kikundi kazi cha Umoja wa Mataifa kinachofuatilia utoaji holela wa adhabu za vifungo ilibaini kuwa kukamatwa kwake pamoja na kuwekwa ndani ilikuwa kinyume na haki haki za binadamu na vilevile  haki za kimataifa kuhusu uhuru wa kisiasa.

Maria Ressa ambaye ni rais wa jopo la wataalamu  lililomchagua Abu Zeid , limesema limetambua ujasiri wake pamoja na azma ya kupigania uhuru wa kujieleza.

Tuzo hiyo itatolewa tarehe Pili mwezi ujao nchini Ghana, wakati wa kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, chini ya kauli mbiu, vyombo vya habari, haki, na utawala wa sheria.

Tuzo ya Guillermo Cano hupatiwa mtu, kampuni ama taasisi kwa mchango  madhubuti wa kutetea, ama kuendeleza  uhuru wa vyombo vya habari hususan wakati wa shida.

Guillermo Cano Isaza mwenyewe ni mwandishi habari wa Colombia ambaye aliuawa mbele ya ofisi za gazeti lake-El Espectador mjini Bogota -Colombia tarehe 17 mwezi disemba mwaka 1986.

Mshindi wa tuzo hiyo hupokea donge nono la dola za kimarekani 25,000.

Tags: Mahmoud Abu Zeid, UNESCO, Guillermo Cano

Audio Credit
Siraj Kalyango
Audio Duration
1'20"
Photo Credit
UN /Martine Perret)