Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utandawazi umezidisha pengo usawa duniani-Guterres

Utandawazi umezidisha pengo usawa duniani-Guterres

Hali ya sasa ya kutokuwa na usawa duniani, kwa njia moja au nyingine, imechochewa na utandawazi.
Ameyasema hayo  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres,wakati akitoa mhadhara kuhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wa pili wa umoja huo, DagHammaeskjold, ambaye aliaga dunia mwaka 1961.
 
Mhadhara huo umefanyika jumapili nchini Sweden ambako wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamekuwa na kikao maalumu cha faragha cha siku mbili. 
Katibu Mkuu katika hotuba yake iliyogusa masuala mbalimbali amesema utandawazi mbali na kuwa na mazuri yake lakini pia una  upungufu.
 
(SAUTI YA GUTERRES)
“Ukweli ni kwamba utandawazi umeongeza kutokuwa na usawa kimchezomchezo,ambapo watu watano katika ulimwengu tunamoishi sasa humiliki mali nyingi sawa na maskini hohehahe wa dunia”
 
Ameongeza kuwa kutokana na hali ya watu wengi kupoteza mengi katika utandawazi, ukiongeza hali ya kuzorota kwa amani na usalama na pia jamii ya kimataifa kushindwa kumudu mienendo ya mwanadamu, hayo na mengineyo yamesababisha mazingira ambayo kwayo watu wameonekana kupunguza  imani yao kwa mifumo ya kisiasa na pia taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa.
 
Amesema hilo ndilo tatizo kubwa wanalokabiliana nalo hii leo 
 
(SAUTI YA GUTERRES2)
 
“ Jinsi ya kujenga imani ya kutosha ambayo itawezesha kuchukua hatua muafaka ya kutanzua migogoro ya wakati wetu”.
 
Ameongeza kuwa moja ya njia ni kufuata yale aliyotaja Dag Hammaeskjold na haja ya kuweka dunia moja kama kitovu cha shabaha zao  ili kuweza kukabiliana vilivyo na matatizo ya dunia wanayokumbana nayo kwa sasa.
 
 
Dag Hjalmar Agne Carl Hammarskjöld alikuwa mwanadiplomasia kutoka Sweden. Lakini pia alikuwa mwanauchumi pamoja na mtunzi wa vitabu. 
Aliwahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa pili tangu Umoja huo uanze, yaani kutoka Aprili mwaka 1953 hadi kifo chake katika ajali ya ndege Septemba 1961. 

Hammarskjöld alichaguliwa kuwa katibu mkuu akiwa na umri wa miaka 47 na inasemekana ndie kinara wa Umoja wa Mataifa mchanga aliewahi kushika wadhifa huo kufukia sasa

Pakua
Audio Credit
Siraj.Kalyango
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
Picha na Moa Haeggblom