Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama waimarika Darfur, waliokimbia waanza kurejea

Usalama waimarika Darfur, waliokimbia waanza kurejea

Pakua

Kuimarika kwa hali ya usalama jimboni Darfur nchini Sudan kumesababisha awamu ya kwanza ya wakimbizi waliosaka hifadhi nchini Chad kurejea jimboni humo wiki hii. 

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema kurejea kwao kunafuatia makubaliano ya mwezi mwaka jana baina ya shirika hilo, serikali ya Sudan na ile ya Chad.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Andrej Mahecic amesema kundi la kwanza la wakimbizi 53 kutoka kambi ya Iridimi, mashariki mwa Chad liliondoka jumamosi na kuwasili Darfur baada ya saa  nne.


Amesema kabla ya kurejea Darfur, wawakilishi wa wakimbizi hao walishakwenda na kukagua hali ilivyo na hatimaye kuamua kwa hiyari yao kurejea nyumbani.

(Sauti ya Andrej Mahecic)

“Wakimbizi wengi wameonyesha nia ya kurejea Sudan miezi ijayo na kadri usalama unavyoimarika jimboni Darfur. Eneo hilo limeshuhudia mwenendo wa wakimbizi na hata wakimbizi wa ndani kurejea nyumbani miaka michache iliyopita. Hii ni kutokana na kuimarika kwa usalama kwenye eneo kubwa la Darfur kufuatia makubaliano kati ya serikali na makundi yaliyojihami.”

Wakimbizi wanaorejea wanasaidiwa usafiri pamoja na mgao wa chakula kwa miezi mitatu, ambao ni usaidizi kutoka shirika la mpango wa chakula duniani, WFP.

Vifa vilizuka Sudan mwaka 2003 na kusababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao na wengine hata kuvuka mipaka na kuingia nchi jirani.

 

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'37"
Photo Credit
Picha: UN Picha / Eskinder Debebe