Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shikamaneni na wana DR Congo- UN

Shikamaneni na wana DR Congo- UN

Pakua

Huko Geneva, Uswisi hii leo imetangazwa kuwa dola bilioni 2.2 zitahitajika mwaka huu wa 2018 ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliosaka hifadhi ndani na nje ya nchi hiyo kutokana na mzozo unaoendelea nchini mwao. 

(Nats)

Sauti ya Grace mwenye umri wa miaka 15 katika video iliyochezwa wakati wa mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu DRCongo. Grace alibakwa na kundi lililojihami wakati wakiwa wameenda kusaka kuni. Sasa ana mtoto na mama yake anafunguka..

(Sauti ya mama mzazi wa Grace)

Fedha zinazoombwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake zitasaidia Grace na wengine wengi kujikwamua kimaisha na pia kupata huduma muhimu pamoja na watoto wao wakati huu ambapo utapiamlo unaelezwa ni wa kiwago cha juu kupita kiasi.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifaya usaidizi wa dharura, Mark Lowcock amesema dola bilioni 2.2 zinazohitajika kwa ajli ya wakimbizi wa ndani na wale waliokimbilia ugenini zinaonekana ni kiasi kikubwa.

(Sauti ya Mark Lowcock)

“Lakini ni sawa na senti 50 kwa siku kwa kila mtu ambaye maisha yake tunataka kuokoa na kulinda. Serikali ya DRC inaonyesha uongozi katika janga hili. Napenda kutangaza pia serikali imeahidi dola milioni 100 katika miezi 18 hadi miezi 24 ijayo kutoka katika mfuko wake zitakazotumika kuwajumuisha katika jamii wakimbizi wa DRC wanaorejea na wakimbizi wa ndani.”

Na ndipo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa video akasisitiza.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Nawasihi nyote hii leo muonyeshe mshikamano wenu na watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”

Jumla ya watu milioni 13 wanahitaji msaada wa kibinadamu huko DR Congo idadi ambayo ni maradufu ikilinganishwa na mwaka jana.

Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
Wakimbizi wa Congo kwa kituo cha transit huko Burundi. (Picha: UNHCR)