Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa amani usigeuzwe "soka"

Mkataba wa amani usigeuzwe "soka"

Pakua

Mkataba wa amani nchini Mali usigeuzwe soka la kisiasa bali utekelezwe ili kufanikisha masuala ya msingi ikiwemo uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hiyo ni kauli ya Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, Mahamat Saleh Annadif wakati akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kujadili masuala kadhaa ya Mali pamoja na mkataba huo wa amani.

Bwana Annadif ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA amesema..

(Sauti ya Mahamat Saleh Annadif)

“2018 ni mwaka wa uchaguzi. Pande husika Mali zisipoteze utambuzi ya kwamba makubaliano ya amani, licha ya uchaguzi, ni lazima yasalie kipaumbele na yasigeuzwe soka la kisiasa.”

Mkuu huyo wa MINUSMA akasihi pande zote nchini Mali pamoja na wananchi kushiriki uchaguzi huo kwa nia njema.

(Sauti ya Mahamat Saleh Annadif)

“Kama inavyotambulika mchakato wa amani ni mgumu lakini baraza hili lazima liwawajibishe pande zilizotia saini ili kuhakikisha mkataba h uo uliotiwa saini hausalii kwenye makaratasi pekee. Ni wakati wa kuondokana na ahadi na kuahidi kuchukua hatua na kuonyesha uzingatiaji wa muda uliopangwa.”

Mali iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Tiéman Hubert Coulibaly ambaye aliwapatiwa wajumbe hakikisho akisema..

(Sauti ya Tiéman Hubert Coulibaly)

“Napenda kusema mbele yenu ya kwamba serikali yangu imeazimia kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa tarehe zilizopangwa na kuhakikisha unakuwa wa wazi, jumuishi na halali. Halikadhalika tumeazimia kuhakikisha uchaguzi unafanyika nchini kote. Ziara ya Waziri Mkuu kwenye maeneo ya kaskazini, ambayo nimetaja awali, ilikuwa ni fursa ya kuonyesha ushirikiano na pande zilizotia saini makubaliano hayo.”

 

 

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
Maafisa wa UNPOL wa kikosi cha Senegal wanapiga doria nchini Mali. Picha MINUSMA / Marco Dormino