Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina hofu na maandamano yaliyopangwa Ijumaa Gaza: Mladenov

Nina hofu na maandamano yaliyopangwa Ijumaa Gaza: Mladenov

Pakua

Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, amesema anafuatilia kwa hofu kubwa maandalizi ya maandamano makubwa ya marejeo yaliyopangwa kufanyika Kesho Ijumaa Ukanda wa Gaza.

Bwana Mladenov ametoa wito kwa vikosi vya Isarael kujizuia kutumia nguvu na kwa Wapalestina kuepuka msuguano wa aina yoyote utakaozusha tafran kwenye uzio wa Gaza. Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, mratibu huyo amesisitiza kuwa maandamano lazima yaruhusiwe kufanyika kwa njia ya amani lakini..

(SAUTI YA STEPHANE DUJARRIC)

“Raia hususani watoto ,lazima walindwe wasiwekwe kwa makusudi katika hatari au kulengwa kwa namna yoyote ile.”

Wahudumu wa misaada ya kibinadamu wanasema, kuna upungufu mkubwa wa madawa muhimu na vifaa vya tiba kwenye vituo vya afya mjini Gaza na hakuna akiba yoyote hivi sasa ya dawa muhimu zilizoorodheshwa na pia hakuna robo ya vifaa vya tiba vinavyohitajika.

Hospitali za Gaza tayari zilikuwa katika hali mbaya kutokana na  tatizo la umeme linaloendelea na upungufu wa dawa na vifaa , sasa Umoja wa Mataifa unasema takriban dola milioni moja zinahitajika haraka ili kusaidia mfumo wa afya wa Gaza kwa ajili ya kununua madawa, vifaa, petrol na vifaa vya maabara katika wiki 6 hadi 8 zijazo.

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'26"
Photo Credit
UN /Loey Felipe