Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwaheri Winnie Mandela umeacha pengo lisilozibika katika haki: Guterres

Kwaheri Winnie Mandela umeacha pengo lisilozibika katika haki: Guterres

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema taarifa za msiba wa mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu na kupinga ubaguzi wa rangi Winnie Madikizela Mandela uliotokea mapema leo umemshitua na kumgusa sana.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stephane Dujarric, Katibu mkuu amemueleezea Winne kuwa ni kioo cha ukombozi na kwamba ni

(SAUTI YA STEPHANE DUJARRIC)

“kiongozi aliyekuwa msitari wa mbele katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini . Alikuwa na sauti yenye nguvu na isiyo na hofu katika mapambano ya kuwa na haki sawa na atakumbukwa daima kama ishara ya upinzani.”

Katibu Mkuu pia ametuma salamu za rambirambi kwa watu, serikali ya Afrika kusini na kwa familia ya Bi Mandela kufuatia msiba huo mzito.

Winnie Mandela ameeaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 katika hospitali ya Netcare Milpark mjini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda maradhi yaliyomfanya kulazwa hospitali mara kadhaa tangu kuanza kwa mwaka huu.

Alikuwa mke wa rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela kwa miaka 38, ikiwemo miaka 27 ambayo Nelson Mandela alikuwa kifungoni kisiwani Robeben mjini Cape Town.

Nelson mandela alitoka jela mwaka 1990 na 1994 akawa rais wa kwanza mwafrika nchini humo. Winnie na Nelson Mandela walitalikiana 1996 na walikuwa na watoto wawili wa kike.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'30"
Photo Credit
UN Photo.