Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twashambuliwa lakini hatukati tamaa- Guterres

Twashambuliwa lakini hatukati tamaa- Guterres

Pakua

Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa wakati huu zinafanya kazi katika mazingira magumu tena yenye hatari kubwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo akihutubia mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hatua za pamoja za kuboresha operesheni hizo.

Ametaja sababu za ugumu kwenye operesheni hizo kuwa ni pamoja na vitisho kutoka kwa magenge yenye silaha, wahalifu na magaidi ambao wana silaha za kisasa tena zenye nguvu.

Ametolea mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati na  Sudan Kusini akisema mbali na vitendea kazi kuwa havitoshi au vilivyopitwa na wakati lakini pia walinda amani wa UN wanalengwa.

(Sauti ya Antonio Guterres)

 “Mwaka jana tulipoteza walinda amani 59 kupitia mazingira ya visa vyenye nia mbaya. Hii ni zaidi ya vifo vya mwaka 2016 ambapo waliofariki waklikuwa ni 34.”

Amesema inafaa kutokuwa na matarajio ambayo si ya ukweli na kufanya hivyo huwa kunaharibu kiungo muhimu cha kulinda amani.

Hata hivyo licha ya shida hizo, Katibu Mkuu pia ameonyesha kufurahishwa kwa na kazi za operesheni za kulinda amani akisema  zimefanikiwa akitoa mfano wa Cambodia, Namibia, El Salvador ambako amesema kutokana na mchango wa Umoja wa Mataifa amani imepatikana baada ya vurugu za muda mrefu.

Na zaidi ya nchi hizo ametaja..

(Sauti ya Antonio Guterres)

 “Afrika magharibi, kwa mfano , Liberia , Sierra Leone na Côte d’Ivoire sasa zina amani na shukrani kwa upande fulani ni kutokana na  mchango wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa. Inatia moyo kuona Cote d’Ivore imewakilshwa leo katika baraza hili na vikosi witatu vya kulinda amani vimerejea nyumbani  baada ya kumaliza vizuri kazi waliyovituma. Hilo ndilo lengo letu kwa kila kazi.”

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'53"
Photo Credit
MONUSCO/Anne Herrmann