Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa na mizozo ni Zinduna na Ambari

Njaa na mizozo ni Zinduna na Ambari

Pakua

Mizozo na njaa kali vyaendelea kuambatana kwenye maeneo kadhaa duniani na kuacha watoto, wanawake, wanaume, vijana kwa wazee hoi bin taaban. Baraza la Usalama lakumbushwa wajibu wake.

Mizozo na njaa, ni mada kuu iliyojadiliwa leo kwenye Baraza la Usalama laUmoja wa Mataifa, wajumbe wakiangazia ni kwa jinsi gani vitendo vya chuki baina ya pande kinzani kwenye migogoro vinachochea ukosefu wa uhakika wa chakula.

David Beasley ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP akihutubia kikao hicho kwa njia ya video kutoka Biel, Uswisi amesema watu milioni 489 duniani wanakumbwa na njaa iliyosababishwa na binadamu.

Bwana Beasley amesema katika kila eneo la vita alilotembelea, watu walikuwa wanaomba kuwepo na amani kama wanavyoomba wapatiwe chakula.

Aliwaeleza wajumbe kuwa hebu wabonge bongo iwapo mtu hafahamu ni wapi atapata mlo ujao wa mtoto wake, mtu huyo anaweza kuchukua hatua ambayo haiwezi kufikirika.

(Sauti ya David Beasley)

“ISIS na makundi ya kigaidi yanataka kutumia chakula kama silaha ya kusajili wanachama wao au silaha ya vita. Tunadhani Baraza la Usalama, Umoja wa Mataifa na wahisani kote ulimwenguni na nchi wanachama tutumie chakula kama silaha ya ujenzi, silaha ya amani, silaha ya kuleta watu pamoja.”

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
2'8"
Photo Credit
Baa la njaa lashuhudiwa nchini Sudan Kusini.(Picha:UNICEF/Sebastian Rich)