Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kweli nyumbani ni nyumbani: IOM DRC

Kweli nyumbani ni nyumbani: IOM DRC

Pakua

Shirika la umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, limepokea msaada wa dola 900,000 kutoka kwa serikali ya Japan ili kuwasaidia watu 200,000 ambao wanaorejea nyumbani, wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi katika jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Shirika hilo linasema wakati hali ya usalama ikianza kutengamaa taratibu, watu wameanza kurejea nyumbani tangu mwishoni mwa 2017, hususani katika eneo la Kasai Kati ambako hadi kufikia leo watu 700,000 wamesharejea. Hata hivyo kwa mujibu wa IOM matukio ya kuvuruga usalama na mivutano ya kijamii inayoendelea inasababisha wimbi jipya la watu kufungasha virago na kutawanywa.

Kutokana na mahitaji fedha hizo za Japan zitafadhili mradi kwenye eneo la mpakani la Kamako ambako watu 200 wanavuka mpaka kila siku kutoka Angola na kurejea nyumbani Kasai, na mradi huo utajikita katika kusaidia maji, usafi na kujisafi (WASH), kutoa huduma za afya, vifaa visivyo chakula, kuelimisha jamii, na kutoa ulinzi hususan dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Tangu kuzuka kwa machafuko 2016, jimbo la Kasai Kati kufikia sasa linahifadhi wakimbizi wa ndani takriban milioni 1.4 kati ya wakimbizi wote wa ndani milioni 4.5 nchini humo.

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'27"
Photo Credit
Raia wa DRC kijijini cha Kasai. Picha: OCHA