Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusikate tamaa mzozo wa Syria- Guterres

Tusikate tamaa mzozo wa Syria- Guterres

Mwaka wa saba wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ukitimu nchini Syria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea machungu yake yanayokumba raia wasio na hatia wakiwemo watoto.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana leo mahsusi kuangazia Syria ambako vita sasa imeanza mwaka wa nane, Katibu Mkuu amesema mwaka 2017 umeshuhudia idadi kubwa zaidi ya watoto wakiuawa.

Na kama hiyo haitoshi, bado maeneo  yamezingirwa, makombora yanaporomoshwa na usaidizi wa kibinadamu  umekumbwa na sintofahamu kubwa.

Amesema azimio namba 2401 la Baraza la Usalama lililotaka kusitishwa kwa chuki baina ya pande kinzani na sitisho la mapigano kwa siku 30 bado halijaweza kuzaa matunda.

Bwana Guterres amesema ingawa kuna maeneo ambako ukali wa mapigano umepungua bado hali si shwari..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hasa katika eneo la Ghouta Mashariki, urushaji wa makombora kutoka angani na ardhini umeshika kasi hata baada ya kupitishwa kwa azimio, na imesababisha vifo vya mamia ya raia, ikiripotiwa idadi ni zaidi ya 1,000.”

Kwa mantiki hiyo amerejelea wito wake kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hatuwezi kukata tamaa kwa maslahi ya raia wa Syria. Natoa wito kwa pande zote kutekeleza azimio namba 2401 nchini kote Syria na Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia kwa njia zote ili litekelezeke. Natoa wito kwa nchi zote zenye ushawishi kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa wa kutekeleza azimio hilo.”

Katibu Mkuu amesema ni matumaini yake kuwa mkutano wa Astana, Uturuki utakaofanyika wiki hii utafungua njia.

 

Pakua

Katibu Mkuu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikuwa anahutubia baraza la usalama la Umoja wa mataifa katika kika maalum kuhusu syria

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'46"
Photo Credit
UNICEF/Khabieh