Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angola msirejeshe wakimbizi wa DRC kwa nguvu

Angola msirejeshe wakimbizi wa DRC kwa nguvu

Hali ya mapigano kwenye eneo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inatishia usalama siyo tu ya wakazi wa eneo hilo bali pia wakimbizi waliorejeshwa kwa nguvu kutoka Angola.

Ukosefu wa usalama umezidi kugubika eneo hilo ambako majeshi ya serikali yanapambana na waasi huku mapigano ya kikabila nayo yakishamiri.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema hali hiyo inatishia kutumbukiza eneo hilo katika ghasia mpya.

UNHCR imenukuu wafanyakazi wake huko Tshikapa, kilometa 60 kutoka mpaka wa DRC na Angola wakisema kuwa ghasia hizo zimesababisha wakimbizi waliorejeshwa kutoka Angola washindwe kurejea kwenye makazi yao.

Wakimbizi walikimbilia Angola ambako katika siku chache zilizopita wakimbizi 530 wamerejeshwa kwa nguvu huku wengine wakisalia kuishi kwenye misikiti na makanisa.

Aikaterini Kitidi, ni msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Aikaterini Kitidi)

“UNHCR inaamini kuwa huu si wakati muafaka kwa wakimbizi kurejea kwa usalama, kwa utu na kwa njia endelevu, kwa kuwa hakuna amani na usalama kwenye makazi yao. Tunaisihi Angola ijizuie na hatua ya kulazimisha wakimbizi wengine zaidi kurejea DRC. Iwapo hali itabadilika tuko tayari kusaidia Angola na DRC kujadili njia ya kurejea kwa hiari.”

Tangu mwezi uliopita, ghasia zimesababisha watu zaidi ya 11,000 kusalia wakimbizi wa ndani ikiwa ni nyongeza ya watu zaidi ya 900,000 ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani tangu mwaka 2016 ghasia zilipozuka eneo la Kasai.

Pakua
Audio Credit
John Kibego
Audio Duration
1'24"
Photo Credit
Picha: UNHCR