Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila Mtoto Awe Hai au Every Child ALIVE

Kila Mtoto Awe Hai au Every Child ALIVE

Pakua

Kiwango cha vifo vya watoto wachanga duniani  hivi sasa bado ni kikubwa na kinatisha, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika ripoti yake mpya iliyotolewa leo.

Kilio hiki huleta nuru tu pale mama anapojifungua akijuwa kuwa mwanae yu hai! Hata hivyo UNICEF katika ripoti yake inasema kuwa uhai huu ni nadra sana kudumu kwa zaidi ya mwezi mmoja kwa watoto wanaozaliwa katika nchi kama vile  Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Somalia, Lesotho, Afghanistan na Sudan Kusini.

Watoto hao hufariki dunia kabla ya kutimiza mwezi mmoja huku watoto wanaozaliwa kwenye nchi kama vile Iceland, Japan na Singapore wakiwa na uhakika wa kuishi kwa asilimia 100.

Miongoni mwa sababu za vifo vya watoto hao ni kuzaliwa njiti, tatizo wakati mama anapojifungua na maambukizi ya magonjwa kama vile vichomi. Nyibol Mayen ni mjamzito kutoka Sudan Kusini anaelezea madhila wanayokumbana nayo..

 (Sauti ya Nyibol Mayen)

“Ninapojifungulia nyumbani, sina msaada. Sina hata pamba, kwa hiyo ni changamoto kubwa. Kama hakuna kiwembe, mwanamke wa kijijini analazimika kuchonga kijiti ili kutumia kukata kitovu cha mtoto.Hizi ni baadhi ya changamoto za kujifungulia nyumbani.”

Sasa UNICEF inazindua kampeni mahsusi iitwayo  Kila Mtoto Awe Hai au Every Child ALIVE, ikilenga kusaka suluhu kwa uhai wa watoto wachanga.

 Willibald Zeck kutoka UNICEF anaelezea kile ambacho wanalenga kupitia kampeni hiyo..

(Sauti ya Willibald Zeck)

 “UNICEF inajikita katika huduma bora ya malezi. Tunachoona wanawake na watoa huduma wamewezeshwa katika nchi mbalimbali. Lakini tatizo bado ni ukosefu wa huduma bora na ndio maana bado nchi nyingi zina shida.Tunatumai kwa kuimarisha uwezo, watu, maeneo na bidhaa tutakuwa tumefikisha pia vifaa katika hospitali zilizo ngazi ya wilaya.”

Audio Credit
Patrick Newman
Audio Duration
2'13"
Photo Credit
© UNICEF/UN0156916/Dicko