Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya watoto wachanga bado kizungumkuti

Vifo vya watoto wachanga bado kizungumkuti

Pakua

Kiwango cha vifo vya watoto wachanga duniani  hivi sasa bado ni kikubwa na kinatisha, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF katika ripoti yake mpya iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo imetaja nchi ambazo ni bora zaidi kuzaliwa ambazo ni pamoja na Japan, Iceland na Singapore huku watoto wanaozaliwa Pakistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Afghanistan wakiwa katika hatari zaidi ya kufariki dunia.

Ripoti inaonyesha kuwa nchi 8 kati ya 10 ambako ni hatari zaidi kuzaliwa ziko barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Sababu za vifo ni pamoja na kuzaliwa njiti, tatizo wakati mama anapojifungua na maambukizi ya magonjwa kama vile vichomi.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta H. Fore amesema ingawa takwimu zinaonyesha kuwa robo karne iliyopita idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ilipungua kwa asilimia 50, bado  kuna tatizo kwa watoto wenye umri wa chini ya mwezi mmoja.

Kwa kutambua hilo, mwezi huu UNICEF inazindua kampeni mahsusi iitwayo  Kila Mtoto Awe Hai au Every Child ALIVE, ikilenga kusaka suluhu kwa uhai wa watoto wachanga.

UNICEF kupitia kampeni hiyo inazitaka serikali, wahudumu wa afya, wahisani, sekta binafsi na familia zichukue hatua kuhakikisha huduma za afya zinapatikana ili kulinda uhai wa watoto hao.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'16"
Photo Credit
UNICEF/UN032140/Mackenzie