Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yaridhia dola milioni 50 kwa ajili ya Yemen

CERF yaridhia dola milioni 50 kwa ajili ya Yemen

Pakua

Umoja wa Mataifa umeridhia dola milioni 50 kwa ajili  ya kuboresha hali ya kibinadamu nchini Yemen.

Fedha hizo zimetoka mfumo wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF ambapo mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa majanga, Mark Lowcock amesema fedha hizo zitaokoa maisha.

Hata hivyo Bwana Lowcock amesema mambo matatu yanapaswa kuzingatiwa ili fedha hizo zitekeleze malengo yake.

Ametaja mosi ni kusitisha mashambulizi ya ardhini na angani ambayo kwa siku za karibuni yamezidi kushamiri, pili bandari zote zisalie wazi bila kufungwa ili shehena za misaada ziweze kuwasilishwa bila vikwazo na tatu michango kutoka kwa wahisani iendelee kuwasilishwa kwa sababu idadi ya wahitaji imeongezeka kutokana na mapigano yaliyoshamiri karibuni.

Mkuu huyo wa OCHA amesema fedha za leo zitahakikisha misaada inawafikia walengwa katika wilaya 27 za Yemen zilizoathirika zaidi ambazo ziko hatarini kukumbwa na njaa.

Nchini Yemen watu zaidi ya milioni 22 wanahitaji misaada ya kibinadamu na milioni 8 kati yao wako hatarini kukumbwa na njaa kali.

Photo Credit
Mvulana mdogo anaendesha tai yake karibu na jengo lililoharibiwa na mikombora huko Saada Yemen. File: OCHA / G.Clarke