Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandamano si uhalifu; Zeid aieleza Iran

Maandamano si uhalifu; Zeid aieleza Iran

Pakua

Chondechonde Iran shughulikieni kwa uangalifu wimbi la maandamano yanayoendelea nchin humo, amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein katika taarifa yake aliyotoa hii leo.

Amenukuliwa na ofisi yake akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuepusha ghasia na vurugu zaidi, ikiwa ni siku moja baada ya Umoja wa Mataifa nao kutoa kauli kupitia naibu msemaji wa chombo hicho.

Sambamba na hilo, Bwana Zeid ametaka serikali ya Iran ichunguze vifo vyote pamoja na majeruhi ambao wameripotiwa hadi sasa akisema anachukizwa sana kwani hadi sasa watu zaidi ya 20 wameuawa akiwemo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 11.

Kamishna Mkuu amesema Iran lazima iheshimu haki na uhuru wa waandamanaji na wale wanaoshikiliwa korokoroni ikiwemo haki yao ya kuishi, usalama na ulinzi.

Sambamba na hilo amesihi mamlaka ziwaachilie huru waandamaji wanaoshikiliwa hovyo kwa kutoa maoni yao wakati wakiandamana kwa amani akisema maandamano ya amani hayapaswi kuwa uhalifu kwani ni mchakato wa demokrasia.

Photo Credit
Mwanafunzi wa Chuo kikuu huko Tehran katika maandamano. Picha: OHCHR