Hali ya kibinadamu Syria bado ni mateso matupu- Mueller
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura, Ursula Mueller, amesema hali bado ni tete nchini Syria kufuatia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa zaidi ya miaka saba sasa.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu Syria, Bi. Mueller amesema mgogoro huo umesababisha mateso makubwa kwa wananchi, vifo vingi kwa raia na huku wengine wakijeruhiwa au kutojulikana waliko.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 13.1 wanahitaji ulinzi pamoja na msaada wa kibinadamu.
Miongoni mwao milioni 6.1 hawana makazi nchini mwao na wengine milioni 5.5 wametorokea nchi jirani.
Bi. Mueller ameliambia Baraza la Usalama kuwa wakati huu mapigano yakiwa yanaendelea ana wasiwasi na maisha ya raia wa kawaida ambao wamejikuta katikati ya mapigano kaskazini Mashariki mwa Syria ambako uhasama unaoendelea unaripotiwa kusababisha vifo pamoja na majeruhi kadhaa.
Takriban watu 60,000 wamerejea mjini humo tangu kumalizika kwa mapigano Oktoba mwaka 2017.
Wakati huo huo, akizungumza kwa njia ya video kutoka mjini Sochi, Urusi ambako mkutano kuhusu Syria unaendelea, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesema
(Sauti ya Staffan de Mistura)
"Tumekubaliana kuunda kamati ya katiba itakayojumuisha serikali, upinzani na washiriki huru ili kuandaa rasimu ya katiba kwa misingi ya azimio la Baraza la Usalama namba 2254. Tuliweza kujumuisha kwenye azimio la mwisho la mkutano wa majadiliano wajibu wa wote kwamba lengo la yote tunayojaribu kufanya ni kutekeleza kikamilifu azimio la Baraza la Usalama.”