Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban watumia gari la wagonjwa kushambulia Kabul

Taliban watumia gari la wagonjwa kushambulia Kabul

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio lililofanyika leo kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul ambako washambuliaji walitumia gari linalofanana na gari la wagonjwa kutekeleza shambulio hilo.

Vyombo vya habari vinaeleza kuwa watu wapatao 95 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika shambulio hilo ambalo kikundi cha Taliban kimekiri kuhusika nalo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA umesema gari hilo pamoja na kufanana na la wagonjwa lilikuwa limewasha king’ora na kulipuka kwenye eneo lenye watu wengi mjini Kabul.

Bwana Guterres kupitia msemaji wake amesema mashambulizi holela dhidi ya raia ni kinyume che sheria za kimataifa na hivyo ametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Ametuma salamu za rambira kwa serikali na wananchi wa Afghanistan huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unashikamana na serikali ya Afghanistan na wananchi wake.

Photo Credit
Taswira ya Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. (Picha:UNAMA/Fardin Waezi)