Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na IOM wanoa ushirika kwa ajili ya uhamiaji

FAO na IOM wanoa ushirika kwa ajili ya uhamiaji

Pakua

Shirika la chakula na kilimo FAO na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM leo wametia saini makubaliano mapya ya ushirika kuhusu suala la uhamiaji na kundi la kimataifa la uhamiaji GMG.

Kundi hilo la GMG likijumuisha mashirika zaidi ya 20 ya Umoja wa Mataifa linatambulika kama chanzo cha msaada wa kiufundi na ushauri kuhusu uhamiaji kwa nchi wanachama na wenyeviti kwa mwaka 2018 ni FAO na IOM.

Makubaliano haya mapya yatatumika kama msingi kwa FAO na IOM kuingiza mtazamo wa kimaendeleo katika miradi ya kimataifa ya uhamiaji kuchagiza umuhimu wa kilimo na maendeleo vijijini katika mtazamo wa uhamiaji.

Pia utaimarisha ushirika katika uelimishaji, kushirikiana utaalamu na ushauri kuhusu kuandaa, kutekeleza na kufuatilia programu zinazopitishwa katika sera za maendeleo ya nchi ikiwemo uhamiaji kisha mikakati hiyo kuendelezwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

IOM inajikita zaidi katika kuboresha usimamiaji wa masuala ya uhamiaji kote duniani kwa kusaidia katika sera, kiufundi , kuzijengea nchi uwezo na masuala ya dharura, wakati FAO itajikita katika kushughulikia vyanzo vinazochagiza uhamiaji usio na mpangilio na kukumbatia uwezekano wa maendeleo yatokanayo na uhamiaji kwa kuwekeza katika uundaji wa ajira vijijini na kuongeza uwezo wa familia za vijijini kujikimu kimaisha.

Photo Credit
Wakimbizi barani Afrika katika maadhimisho ya siku ya wahamiaji(MAKTABA). Picha: IOM