Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna aliyeshinda au kushindwa sote ni Waliberia:George Weah

Hakuna aliyeshinda au kushindwa sote ni Waliberia:George Weah

Pakua

Nderemo na vifijo vilitawala leo kwenye uwanja wa mji mkuu Monrovia nchini Liberia wakati wa hafla ya kuapishwa Rais mpya wa nchi hiyo George Weah. Akizungumza baada ya kuapishwa mbele ya kadamnasi iliyofurika uwanjani hapo na uwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambao wiki chache zijazo utafunga milango ya mpango wake wa kulinda amani nchini humo baada ya kuwepo kwa miaka 15, mwana kabumbu huyo nyota wa zamani amesema

(SAUTI YA GEORGE WEAH CUT 1)

“Nimetumia miaka mingi ya maisha yangu kwenye uwanja wa kandanda, lakini leo hisia nilizonazo hazilinganishwi na chochote. Nawahakikishia tutakapomaliza hakutakuwa na mshindi na aliyeshindwa, leo hii sote tunavaa jezi ya Liberia.”

Weah ambaye anamrithi Bi Ellen Johnson sirleaf Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo baada ya miaka 70, ameushukuru mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMIL kwa juhudi zake za kurejesha amani na usalama baada ya vita mbili za wenyewe kwa wenyewe zilizodumu kwa miaka 14 tangu 1989 hadi 2003 akisema

(SAUTI YA GEORGE WEAH CUT 2)

“Tunasimama na misingi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, wakati tulipokuwa katika siku za kiza Umoja wa Mataifa ulisimama nasi, mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ulihakikisha unadumisha amani katika mipaka yetu kwa zaidi ya muongo, na punde utadhihirisha imani yao kwetu kwa kubadili jukumu lake kutoka ulinzi wa amani na kugeukia programu za Umoja wa Mataifa ambazo zitaendelea katika sekta muhimu kama elimu, afya, na kilimo.”

Aliyeongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika hafla hiyo ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Afrika Magharibi  na Sahel Bwana Mohammed ibin Chambas na msaidizi wa Katibu Mkuu katika operesheni za ulinzi wa amani Perations Bintou Keita.

Kuanzia tarehe 31 Machi nafasi ya mpango wa UNMIL itachukuliwa na timu ya Umoja wa Mataifa nchini Liberia.

Photo Credit
Rais mpya wa Liberia L George Weah (katikati) na rais wa zamani wa nchi hiyo Ellen Johnson Sirleaf (kulia) wakati wa hafla ya kuapishwa kwa weah katika uwanja wa SKD mjini Monrovia, Liberia 22 Januari 2018. Picha na: UN info/Pascal Sim