Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres apongeza hatua kati ya serikali ya Congo na waasi

Guterres apongeza hatua kati ya serikali ya Congo na waasi

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua iliyofikiwa huko Jamhuri ya Congo baada ya serikali na Frédéric Bintsamou ambaye hujulikana zaidi kama mchungaji Ntumi kutia saini makubaliano ya kusitisha chuki kati yao.

Makubaliano hayo yalitiwa saini mwishoni mwa wiki ambapo Bwana Guterres amesema ni matumaini yake kuwa yatawezesha suluhu ya kudumu na ya amani kwenye mzozo unaoendelea kwenye eneo la Pool.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kusaidia  kuunga mkono pande hizo ili waweze kutekeleza na hivyo kumaliza hali ya mbaya ya kibinadamu kwenye enee hilo lililo kusini mwa mji mkuu, Brazaville.

Pande mbili hizo zimekuwa katika mzozo tangu mwezi Aprili 2016 baada ya Mchungaji Ntumi kuongoza uasi wa kupinga kuchaguliwa tena kwa Denis Sassou Nguesso kuwa rais wa Jamhuri ya Congo.

Photo Credit
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Picha: UM