Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni binafsi za ulinzi zatishia utulivu wa Ghana

Kampuni binafsi za ulinzi zatishia utulivu wa Ghana

Pakua

Ghana kuweni macho na kampuni binafsi za ulinzi ambazo siyo tu idadi yao imeongezeka kama uyoga bali pia zinaweka upenyo wa askari mamluki.

Hiyo ni kauli iliyotolewa na wajumbe wa kikundi kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya askari mamluki baada ya ziara yao ya siku nane huko Ghana.

Wataalamu hao wameonyesha wasiwasi wao juu ya uwepo wa vikundi 400 vya ulinzi visivyo halali licha ya kuwepo kwa sheria za kudhibiti.

Kampuni hizo zinaajiri zaidi ya watu 450,000 huku idadi ya polisi ni 33,000.

Cha kutia hofu zaidi askari hao wa kampuni binafsi wakipatiwa jina la askari wa miguu wana silaha licha ya kwamba wengi wao hawana mafunzo sahihi.

Wataalammu hao wameenda mbali zaidi wakisema baadhi ya askari hao hujihusisha na vyama vya siasa na hatimaye kuleta ghasia wakati wa chaguzi.

Kwa mantiki hiyo wametaka serikali ya Ghana iangalie upya sheria zake ili kudhibiti hali ya sasa ili kuendeleza amani na utulivu kwa nchi hiyo ijulikanayo kama kijito cha amani.

Ripoti ya wataalamu hao itawasilishwa mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwaka 2018.

Photo Credit
Bendere ya Ghana. Picha: UM/Loey Felipe