FAO na WFP kwa pamoja kukabiliana na njaa DRC

FAO na WFP kwa pamoja kukabiliana na njaa DRC

Pakua

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo FAO, na la mpango wa chakula WFP yamekusanya nguvu ili  kukabiliana na tatizo la njaa katika eneo la Kasai Kuu huko jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Alexis Bonte ambaye ni mwakilishi wa muda wa  FAO amesema watatumia kiasi cha dola milioni 10 zilizotolewa na serikali ya Ubelgiji ili kuboresha maisha ya raia laki moja ambao ni wakimbizi wa ndani katika migogoro ya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la Kasai.

Naye Claude Jibidar ambaye ni mwakilishi wa WFP DRC amesema mpango  huo si wa kusaidia chakula tu bali kujengea uwezo sekta ya kilimo nchini humo ili iweze kutatua tatizo la hapo baadaye.

Katika mpango huo, WFP imesema itajikita na ugawaji wa vyakula kama mahindi, mbogamboga, mafuta ya kupikia na chunvi huku FAO ikijikita na pembejeo za kilimo kama vile mbolea na pia mbegu za miti  ya matunda na mimea mbalimbali.

Mashirika hayo yamesema migogoro ya huko Kasai Kuu imeathiri jamii ya zaidi ya watu milion3.2 inayojulikana kwa kilimo cha mahindi nchini DRC, hususan wanawake, watoto na wazee.

Photo Credit
Wakulima nchini DRC wamwagilia maji mimea. Picha: FAO