Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutolinda suluhu ya mataifa mawili kunadhoofisha wasimamizi na kuimarisha wanamgambo:Mladenov

Kutolinda suluhu ya mataifa mawili kunadhoofisha wasimamizi na kuimarisha wanamgambo:Mladenov

Pakua

Umoja wa Mataifa umerejelea kauali yake kwamba Yerusalemu ni suala la mwisho kuhusu Mashariki ya Kati ambalo linapaswa kushughulikiwa kupitia mazungumzo ya amna kwa ana baina ya Israel na Palestina.

Hayo yamesemwa leo kwenye kikao cha baraza la Usalama na mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa mani ya Mashariki ya Kati Nikolai Mladenov alipotathimini ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa azimio namba 2334 kuanzia Septemba 20 hadi Desemba 18 mwaka huu.

Mladenov amesema kipindi kilichojumuishwa kwenye ripoti hiyo hakijaonyesha hatua zozote chanya za kusongesha mbele mchakato wa amani na pande zote bado zimegawaika mapande.

Mladenov akizungumzia uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuutambua rasmi mji wa Israel kama mji mkuu wa taifa la Israel amesema

(SAUTI YA NIKOLAI MLADENOV)

"Umoja wa Mataifa una nia ya kuona Yerusalemu kama ni suala la mwisho la kutatuliwa kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande mbili na kwa misingi ya maazimio ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu, kwa kuzingatia masuala ya halali ya Wapalestina na Israeli. "

image
Wajumbe wa baraza la usalama kwenye mkutano wa kujadili matumizi ya silaha za kemikali kwenye mji wa Khan Shaykhun nchini Syria. Picha: UM/Rick Bajornas
Azimio namba 2334 linathibitisha wito wa Israeli wa kukomesha haraka na kukamilika kwa shughuli zote za ujenzi wa makazi katika eneo linalokaliwa la Palestina ambalo ni pamoja na Yerusalemu ya Mashariki. Mladenov amesema hatua hizi hazikuchukuliwa katika kipindi cha ripoti hii kwani makazi mapya ya walowezi 1200 katika eneo linalokaliwa la Wapalestina yaliidhinishwa

(SAUTI YA NIKOLAI MLADENOV)

“napenda kusisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unachukulia shughuli zote hizo za makazi ni haramu chini ya sheria za kimataifa na ni kikwazo kikubwa cha amani.”

Ameongeza kuwa hali ya machafuko imekuwa mbaya zaidi tangu Desemba 6 baada ya Marekani kutangaza kuutambua mji wa Yerusalemu kama mji mkuu wa taifa la Isarel.

Misri imewasilisha mswada wa kutaka kura ipigwe tena ya azimio 2334 kupinga hatua hiyo ya Marekani ambayo mbali ya kuutambua mji wa Yerusalemu kuwa makao makuu ya Israel inataka kuhamisha ubalozi wake kutoka Telaviv kwenda Yerusalem. Hata hivyo balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameweka bayana nia ya nchi yake katika kura hiyo.

image
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley akiwa kwenye kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa New York. Picha na UN/Evan Schinller
(SAUTI YA NIKKI HALEY)

“Kwenye mkutano huu sitopoteza muda wa baraza keelezea wapi nchi huru itaamua kuweka ubalozi wake na ambapo tuna kila haki ya kufanya hivyo, Nitazungumzia suala ambalo ni la dharura, Desemba 2016 Marekani iliamua kutopiga kura na kuacha azimio hilo kupita, endapo tutapewa tena fursa ya kupiga kura dhidi ya azimio namba 2334 nitasema kwa uhakika kwamba Marekani itapiga kura ya hapana, tutatumia kura yetu ya turufu.”

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya mswada wa azimio kupigiwa kura na matokeo kutangzwa

(SAUTI YA RAIS WA BARAZA LA USALAMA)

“Matokeo ya kura ni kama ifuatavyo , wajumbe 14 wameunga mkono na kura moja imepinga, hivyo mswada wa azimio hakupitishwa kutokana na kura ya turufu ya mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama.”

Mladenov amehitimisha kwa kusema kwamba kukosekana kwa hatua za kulinda mustakhbali wa uwezekano wa kuwa na mataifa mawili na kuunga mkono taifa la Palestina kutadhoofisha wasimamizi na kuimarisha wanamgambo.

Photo Credit
Picha: UN/Eskinder Debebe