Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Darfur walioko CAR waanza kurejea nyumbani:UNHCR

Wakimbizi wa Darfur walioko CAR waanza kurejea nyumbani:UNHCR

Pakua

Wakimbizi wa Sudan waliokuwa kwenye kambi za Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, wameanza kurejeshwa kwa hiyari nyumbani kufuatia uzinduzi wa zoezi hilo unaondeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR juma hili.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi, Barbar Baloch zaidi ya wakimbizi 230 wamewasili kwenye uwanja wa ndege wa Nyala nchini Sudan wiki hii kwa kutumia ndege 66 za UNHCR ambazo zinatarajiwa kuwarejesha nchini humo wakimbizi 1500 kabla ya mwaka huu kumalizika.

Karibu wakimbizi 3500 walikimbia jimbo la Darfur Kusini na kwenda CAR mwaka 2007 wakati wa vita baina ya vikosi vya jeshi la Sudan na makundi ya waasi yenye silaha.

Wakiwa nchini CAR wakimbizi hao wamekuwa wakihifadhiwa kwenye kambi za Pladama Ouaka karibu na jimbo la Bambari.  Na sasa wengi wa wakimbizi hao wanarejea nyumbani kwao kwenye vijiji vya Dafag Darfur Kusini.

UNHCR inashirikiana na serikali ya Sudan na CAR kufanikisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuwapa fungu la fedha na usaidizi mwingine kuwasaidia kuanza upya maisha yao.

Takriban watu milioni mbili ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan na wengine zaidi ya 650,000 ni wakimbizi katika nchi jirani zikiwemo Chad na Sudan Kusini.

Photo Credit
Halima Ibrahim na familia yake ni miongoni mwa wakimbizi wa kwanza wa Sudan ambao wanarudi nyumbani baada ya miaka kumi ya ukimbizini CAR. Picha: © UNHCR / Ahmed Dotum