Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.7 zahitajika kusaidia wananchi wa Sudan Kusini

Dola bilioni 1.7 zahitajika kusaidia wananchi wa Sudan Kusini

Pakua

Mzozo nchini Sudan Kusini ukiingia mwaka wa nne, zaidi ya dola bilioni 1.7 zahitajika ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu kwa nchini humo kwa mwaka 2018.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini humo Alain Noudéhou ametangaza kiwango hicho hii leo kwenye mji mkuu, Juba akisema mpango huo unalenga watu milioni 6 walioathiriwa zaidi na mzozo, kupoteza makazi, njaa na kudorora kwa uchumi.

Amesema ombi hilo lina mipango inayoangazia zaidi ulinzi wa makundi yaliyo hatarini ambayo ni wanawake na watoto wakati huu ambapo mahitaji ya misaada yanaongezeka kutokana na ukosefu wa uhakika wa chakula, utapiamlo na mapigano.

Kwa mantiki hiyo wakipata fedha hizo Bwana Noudéhou amesema wataweza kutoa misaada inayohitajika, mathalani watoto kwenda shuleni na wengine wengi kuepushwa na magonjwa huku wananchi wakijipatia uwezo wa kujikwamua kiuchumi.

Fedha hizo zilizoombwa zitatumika kwenye miradi itakayotekelezwa na mashirika ya miaka 167 ikiwemo 95 ya kiraia, 61 ya kimataifa na 11 ya Umoja wa Mataifa.

Tangu mzozo uanze nchini Sudan Kusini mwezi disemab mwaka 2013, takribani watu milioni 4 wamekimbia makazi yao, ikiwemo milioni 1.9 ambao ni wakimbizi wa ndani na milioni 2.1 wamekimbilia nchi jirani.

Photo Credit
Wakimbizi wa ndani wa Sudan Kusini.(Picha:UNMISS)