Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yavunja rekodi, wahisani 36 waahidi dola milioni 383 kwa 2018:

CERF yavunja rekodi, wahisani 36 waahidi dola milioni 383 kwa 2018:

Pakua

Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF umevunja rekodi ya mapato kwa mwaka 2017 wakati wahisani walipotoa ahadi zaidi za msaada wa fedha kwa mwaka 2018.

Wakati wa mkutano mkutano wa ngazi ya juu wa ahadi za msaada kwa ajili ya mwaka 2018 uliofanyika wiki hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani , wahisani 36 wameahidi dola milioni 383 kwa mfuko wa CERF ili kuhakikisha msaada wa dharura wa kibinadamu unawafikia wahitaji popote na wakati wowote janga linapozuka.

CERF pia imefanikiwa kuvunja rekodi ya mapato kwa mwaka 2017 baada ya kufikia dola milioni 504 kufuatia ahadi zaidi zilizotolewa na wahisani katika mkutano huo.

Kwa kusisitiza jukumu muhimu la CERF wakati watu wanapojikuta wamekwama katika zahma , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza kutenga dola milioni 100 kutoka kwenye mfuko huo  mwaka huu 2017 kwenda kwenye majanga tisa ya dharura ambayo yametelekezwa ambako mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu .

Maeneo hayo ni pamoja na Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Eritrea, Haiti, Mali, Pakistan, Ufilipino, Tanzania na Uganda.

Photo Credit
Bango la mkutano wa ngazi ya juu wa ahadi za usaidizi kwa CERF kwa ajili ya mwaka 2018. Picha na CERF