Watoto milioni 17 wanavuta hewa yenye sumu duniani:UNICEF

6 Disemba 2017

Takribani watoto milioni 17 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja wanaishi katika maeneo ambayo hewa chafuzi ni mara sita zaidi ya kiwango cha juu cha kimataifa na kuwasababisha kuvuta hewa yenye sumu ambayo huweka maendeleo ya ubongo wao hatarini.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF iliyotolewa leo, ikiongeza kuwa zaidi ya robo tatu ya watoto hao ambao ni jumla ya milioni 12 wanaishi katika nchi za Asia Kusini wakifuatiwa na Asia Mashariki na Pacific ambako kuna watoto milioni 4.3 wanaovuta hewa yenye sumu.

Taarifa hiyo iliyopewa kichwa “Hatari hewani:Jinsi gani hewa chafuzi inavyoweza kuathiri maendeleo ya ubongo wa watoto”, imeanisha kwamba kuvuta baadhi ya hewa chafu kunaweza kuharibu mishipa ya ubongo na kuathiti uwezo wa maendeleo ya kutambua vitu.

Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Athony Lake amesema hewa hiyo yenye sumu sio tuu inaathiri ukuaji wa mapafu ya mtoto bali inaweza kuzuru mojakwamoja ubongo wa mtoto na kuuweka njia panda mustakhbali wa maisha yake.

Hivyo amesisitiza kuwa kuwalinda watoto dhidi ya hewa yenye sumu kuna faida sio kwa mtoto tu bali kwa jamii nzima, hasa kwa kupunguza gharama za huduma za afya, kuongeza uzalishaji na kuwa na mazingira bora yenye hewa safi kwa wote.

Amezichagiza nchi kuchukua hatua muafaka sasa ili kuokoa maisha ya watoto hao na mustakhbali wao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud