Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhakika wa chakula na lishe ni changamoto kubwa Asia na Ulaya:FAO

Uhakika wa chakula na lishe ni changamoto kubwa Asia na Ulaya:FAO

Pakua

Baadhi ya nchi za Ulaya na Asia ya Kati ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika zaidi na  mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo imesababisha uharibifu wa mazao, misitu na pia kuathiri sekta ya ufugaji na uvuvi.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyozinduliwa leo na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO yenye kichwa “Kuhakikisha uhakika wa chakula kupitia njia bora za usimamizi wa rasilimali za asili kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi”.

Ripoti hiyo inasema ingawa nchi nyingi katika kanda hizo zimetambua umuhimu wa kukabiliana na changamoto zitokanazo na lishe duni na kuongeza jitihada za kuhakikisha uhakika wa chakula ili kuboresha ustawi wa wananchi wao, mafanikio katika sera na programu za lishe yanafaa kwenda sambamba na mipango ya maendeleo kama vile ulinzi wa jamii, maendeleo ya vijijini na elimu ya lishe, hasa kwa kuzingatia sababu za msingi zinazosababisha utapiamlo.

Halikadhalika ripoti hiyo imesema mahitaji ya chakula katika kanda hizi yameongezeka huku ukuaji wa miji ukifanyika kwa kasi. Wakati huo huo, mifumo mingi ya uzalishaji katika kanda hizi tayari haiwezi kuboreshwa,  hivyo kufikia uhakika wa chakula katika hali hii itahitaji uwekezaji zaidi katika kilimo, mnepo mkubwa na matumizi bora ya rasilimali za asili.

Pia ripoti inasisitiza umuhimu wa kupunguza hasara ya chakula, ikisema kuwa zaidi ya asilimia 30 ya mazao kote duniani yanatupwa. Kwa kupunguza hasara ya chakula, FAO inasema shinikizo kwenye mazingira litapungua, uzalishaji wa gesi chafuzi utapungua, kutakuwa na ufanisi zaidi katika sekta ya kilimo na uhakika wa chakula na lishe utaimarika.

FAO imeongeza kuwa kwa kuzingatia hatua zilizopitishwa ili kufikia ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, ni nchi chache tu katika kanda hizO ambazo zina mifumo ya sera inayozingatia nguzo zote nne za uhakika wa chakula ambazo ni : Uwepo wa chakula, Upatikanaji, matumizi na ustawi.

Photo Credit
Wakulima Uzbekistan. Picha: FAO