Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapiganaji mamluki wanaelekea Libya na Yemen- Voronkov

Wapiganaji mamluki wanaelekea Libya na Yemen- Voronkov

Pakua

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kujadili wapiganaji mamluki wanaojiunga na vikundi vya kigaidi, jambo ambalo linatishia amani na usalama duniani.

Akihutubia kikao hicho, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili ugaidi Vladimir Voronkov amesema suala la wapiganaji mamluki kutumikia vikundi vya kigaidi ni jambo gumu na linalobadilika kila uchao.

Amewapatia wajumbe takwimu zinazoonyesha makadirio kwamba wapiganaji zaidi ya elfu 40 kutoka zaidi ya mataifa 110 wamejiunga na vikundi vya kigaidi vinavyopigana huko Syria na Iraq.

Bwana Voronkov amesema kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali kukabili vitendo vya mamluki kujiunga na vikundi vya kigaidi, pamoja na kushindwa kijeshi kwa magaidi katika baadhi ya nchi, hivi sasa wapiganaji hao wa kigeni wanahamia Libya, Yemen na Afghanistan ambako wanachochea zaidi migogoro.

Amesema sambamba na wanaosaka hifadhi kwingineko, wengine wamerejea nyumbani ambako nako wanaendesha mashambulizi kwenye nchi zao na hata kusajili wapiganaji wapya kwa lengo hilo.

(Sauti ya Vladimir Voronkov)

"Wapiganaji wa kigeni ambao wanarejea nyumbani kwao wanaleta changamoto kubwa bila suluhu yoyote. Suluhu ya haraka inayoshawishi inakuwa pengine kuwasweka wote gerezani au hata kuwazuia wasirejee nyumbani. Lakini kuzingatia kwa umakini sheria za kimaaifa ni muhimu ili kuzuia vitisho vitokanavyo na wapiganaji wa kigeni.”

Kwa mujibu wa Voronkov hivi sasa nchi zimeimarisha mifumo ya kisheria na mifumo ya mahakama ili kuchukua hatua dhidi ya vitisho vitokanavyo na wapiganaji wa kigeni.

Photo Credit
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili ugaidi Vladimir Voronkov . (Picha:UN/Eskinder Debebe)