Uchaguzi mkuu DRC sasa kufanyika disemba mwaka 2018

Uchaguzi mkuu DRC sasa kufanyika disemba mwaka 2018

Pakua

Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CENI, imetangaza kuwa uchaguzi mkuu nchini humo sasa utafanyika mwezi disemba mwakani 2018 badala ya mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Radio  Okapi ambayo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO imemnukuu Rais wa CENI Corneille Nangaa akitangaza mjini Kinshasa kuwa uchaguzi wa rais, wabunge na majimbo utafanyika tarehe 23 disemba mwakani.

Matokeo ya awali ya rais yatatangazwa tarehe 30 disemba 2018 huku matokeo kamili yakitarajiwa tarehe 9 Januari mwaka 2019.

Bwana Nangaa amesema rais mteule ataapishwa tarehe 12 Januari akisema kuwa ratiba ya uchaguzi ambayo wametangaza imezingatia misingi inayotakiwa na pia inalenga kupunguza gharama.

Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwaka huu.

Hata hivyo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC, Maman Sidikou alisema kuna uwekezano uchaguzi huo hautafanyika kutokana na sintofahamu ya kisiasa inayoendelea nchini humo.

Photo Credit
Wafanyakazi wa CENI DRC waendelea kusajili wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi ujao. Picha: MONUSCO