Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yaanza kusajili wakimbizi nchini humo

Ethiopia yaanza kusajili wakimbizi nchini humo

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limekaribisha hatua ya Ethiopia ya kuanza kusajili wakimbizi ambapo wanaweza kusajili taarifa zao za vizazi, vifo, ndoa na hata talaka kwenye mamlaka za kitaifa.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Ethiopia kwa wakimbizi kupatiwa fursa hiyo na inafuatia marekebisho ya sheria yaliyofanyika nchini humo.

Katika uzinduzi leo, wakimbizi 11 walipewa vyeti katika ofisi za usajili wa kiraia kwenye mji mkuu Addis Ababa ambapo pia watoto wapatao 70,000 waliozaliwa nchini Ethiopia katika miaka kumi iliyopita watapatiwa vyeti vya kuzaliwa.

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF  pamoja na UNHCR walishirikiana na serikali katika maandalizi ya sheria hiyo na ni moja ya ahadi tisa ambazo serikali zilipitisha wakati wa mkutano wa viongozi kuhusu uhamiaji uliofanyika New York, Marekani mwezi Septemba mwaka jana.

Hatua nyingine zilizopendekezwa ni kupatia wakimbizi fursa za ajira, kuimarisha upatikanaji wa elimu, kuruhusu idadi kubwa ya wakimbizi hususan wale wa muda murefu kukaa nje ya kambi.

Hivi sasa Ethiopia inahifadhi zaidi ya wakimbizi 883,000 wengi wao wakitoka Sudan Kusini, Somalia na Yemen.

Photo Credit
Ariat Ochocka Odulla ambaye mwanae mvulana wa miaka 18 ni miongoni mwa wakimbizi watoto wa kwanza kupata cheti cha kuzaliwa cha Ethiopia.(Picha:UNHCR/Diana Diaz)