Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 12,000 wa Rohingya wakimbilia Bangladesh kila wiki-UNICEF

Watoto 12,000 wa Rohingya wakimbilia Bangladesh kila wiki-UNICEF

Pakua

Mazingira duni na magonjwa vinatishia maisha ya watoto zaidi ya 320,000 ambao ni wakimbizi wa Rohingya walioingia Kusini mwa Bangladesh tangu mwishoni mwa mwezi Agosti wakiwemo wengine elfu 10 waliovuka mpaka kutoka Myanmar katika siku chache zilizopita na kila wiki wanaingia 12,000.

Hayo ni kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Anthony Lake akiongeza kwamba watoto wengi wakimbizi wa Rohingya walioko Bangladesh wameshuhudia ukatili wa hali ya juu nchini Myanmar hali ambayo hakuna mtoto anayepaswa kuiona na wote wameathirika.

Ameongeza kuwa watoto hawa wanahitaji haraka chakula, maji safi na chanjo ili kuwalinda na maradhi yanayolipuka katika hali za dharura kama inayowakabili. Pia amesema wanahitaji msaada wa kisaikolojia ili kuyakabili yote yaliyowasibu, wanahitaji ushauri nasaha kwani mgogoro huu unapokonya utoto wao na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhakikisha haupori pia mustakhbali wao.

UNICEF inasema wakimbizi wengi wanaishi katika hali ya mrundikano, bila huduma za usafi, na licha ya kuongezeka juhudi za kimataifa za misaada , mahitaji ya watoto mengi hayajatimizwa.

Photo Credit
Mohammed Yasin mwenye umri wa miaka 8, ni miongoni mwa watoto waRohingya wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi huko Bazar ya Cox. Picha: © UNICEF / UN0135698 / Brown