Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya raia wa Afghanistan kwa mwaka 2017 vyakaribia kuvunja rekodi

Vifo vya raia wa Afghanistan kwa mwaka 2017 vyakaribia kuvunja rekodi

Pakua

Vifo vya raia nchini Afghanistan kwa miezi tisa ya kwanza kwa mwaka huu vinakaribia kuvunja rekodi sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mapigano ya ardhini.

Ripoti ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa  wa usaidizi nchini Afghanistan, UNAMA imesema kuanzia  Januari mosi hadi Septemba 30 mwaka huu wa 2017, raia 2,640 waliuawa na wengine 5379 walijeruhiwa.

Ingawa takwimu zinaonyesha idadi ya majeruhi imepungua ikilinganishwa na mwaka 2016, bado idadi ya waliopoteza maisha imeongezeka.

UNAMA inasema vifo  vingi vinavyotokea nchini Afghanistan vimesababishwa na mashambulizi ya kujitoa muhanga wanapotumia vilipukaji vya kutengeneza hususani maeneo ya Kabul, Helmand, Nangarhar, Kandahar, na Faryab .

Ujumbe wa UNAMA huandaa ripoti zake  kwa mujibu wa mamlaka yake chini ya  azimio namba 2274 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  la mwaka 2016 la kufuatilia hali ya wananchi, kuratibu jitihada za kuhakikisha ulinzi wao, kukuza uwajibikaji, na kusaidia katika utekelezaji kamili wa uhuru wa msingi na masharti ya haki za binadamu.

Photo Credit
Picha UNAMA / Fardin Waezi