Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkazo zaidi wahitajika kuzuia ukatili dhidi ya watoto vitani :Gamba

Mkazo zaidi wahitajika kuzuia ukatili dhidi ya watoto vitani :Gamba

Pakua

Kuna haja ya kusisitiza kuzuia na kukomesha ukatili dhidi ya watoto hususani mauaji na kujeruhiwa kote ulimwenguni.

Wito huo umo katika ripoti ya mwaka 2016 kuhusu watoto na vita vya silaha ambayo imetaja kuwa watoto zaidi ya 8000 waliuawa kwenye maeneo yaliyoghubikwa na mizozo mwaka jana .

Akichambua yaliyomo katika ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani Bi virginia Gamba mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kwenye maeneo yanayokabiliwa na vita vya silaha amesema ripoti hiyo ni nyenzo muhimu katika kuzuia ukatili huo.

Watoto katika maeneo ya vita nchini Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Iraq, Somalia, Sudan kusini, Syria na Yemen, wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa haki usiokubalika. Mbali ya kuuawa na kujeruhiwa wanashinikizwa kuingia vitani, shule wanazosomea kusambaratishwa na kuwaacha watoto hao bila mustakhbali bora wa maisha yao.

Ripoti hiyo imeorodhesha visa 4000 vilivyothibitishwa vya ukiukwaji uliofanywa na vikosi vya serikalina na zaidi ya 11,500 na makundi mengine katika nchi 20 kote duniani. Bi Gamba ameongeza kuwa katika kuzuia watoto kuwa wahanga

(SAUTI YA GAMBA1)

“Ripoti hii sasa inatumika kama nyenzo ya kutoa onyo. Kwa kushirikisha wadau wote na kushughulikia ukiukwaji , tunafanya kazi pamoja kuzuia ukiukwaji na kuboresha hali mbaya ya watoto waliojikuta katikati ya mizozo ya silaha  ili waweze kuwa watoto kama inavyopaswa na sio kuwa wahanga wa vitendo vya kikatili. Kushirikisha pande zote katika mizozo kunaendelea na hivyo kuifanya ripoti hii kuwa nyenzzo muhimu ya kuzuia.”

Ametaja vitu vingine vilivyomo kwenye ripoti ambavyo ni changamoto katika vita dhidi ya ukatili kwa watoto kuwa ni kunyimwa fursa za masauala ya kibinadamu kwa raia, kuongezeka kwa makundi ya wanagambo yenye silaha, na muungano wa vikosi vya kigeni katika maeneo yenye vita.

Photo Credit
Bi virginia Gamba mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto. Picha: UM/Cia Pak