Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warundi mliokimbilia nje karibuni mrejee nyumbani:Nyamitwe:

Warundi mliokimbilia nje karibuni mrejee nyumbani:Nyamitwe:

Pakua

Hali ya Burundi imetengamaa na ni wakati muafaka kwa raia waliokimbilia nchi jirani na nchi za nje kurejea nyumbani. Wito huo umetolewa leo na waziri wa mambo ya nje wa Burundi Alain Aimé Nyamitwe akihutubia mjadala wa wazi wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa New York Marekani.

Nyamitwe amesema pamoja na changamoto zingine za kiuchumi kama yalivyo mataifa mengine ya Afrika , nchi hiyo imejitahidi kusuhulisha hali ya mvutano wa kisiasa uliojitokeza mwaka 2015 na kusabababisha watu wengi kukimbia nchini humo.

Amewaomba raia wa Burundi walio wakimbizi nchi jirani na hata nje ya bara la Afrika kurudi nyumbani ili kusaidia kulijenga taifa hilo.

Amezishukuru nchi jirani ikiwemo Tanzania , Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa kubeba mzigo wa wakimbizi kutoka nchini humo. Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na hususani shirika la Umoja wa Mataifa UNHCR kusaidia mchakato wa kuwarejesha nyumbani kwa hiyari wakimbizi hao.

Bwana Nyamitwe akuzungumzia pia hatua zilizopigwa na Burundi katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDG’s akisema wamepiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya, mazingira kwa kuweka mikakati ya kukbiliana na mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia.

Na katika suala la ugaidi amesema hiyo ni changamoto ya kimataifa inayohitaji suluhu ya kimataifa.

Ameongeza kuwa Burundi inaungana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kuhakikisha usalama wa kimataifa. Amepongeza juhudi za muungano wa Afrika katika kuhakikisha bara hilo halisalii nyuma katika maendeleo akitaja kuwa Burundi itahakikisha ajenda ya mwaka 2063 ya Muungano wa Afrika inang’aa nchini mwake.

Photo Credit
Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Alain Aimé Nyamitwe akihutubia mjadala wa wazi wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani. Picha na UN Web TV.