Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia yakabiliwa na uhaba wa viua vijasumu- WHO

Dunia yakabiliwa na uhaba wa viua vijasumu- WHO

Pakua

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema kuna uhaba mkubwa wa dawa mpya za viua vijasumu au antibayotiki wakati huu ambapo kuna usugu wa dawa za kutibu magonjwa kama vile Kifua Kikuu au TB.

Ripoti ya WHO iliyotolewa hii leo imesema hali hiyo imebaini baada ya kuonekana kuwa hata dawa aina ya viua vijasumu ambazo ziko kwenye majaribio si mpya bali ni maboresho tu ya dawa zinazotumika hivi sasa na kwamba ni kwa ajili ya suluhu ya muda mfupi.

Akizungumzia taarifa hizo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuna umuhimu wa haraka wa kuwekeza kwenye utafiti na maendeleo kwa ajili ya dawa mpya dhidi ya magonjwa kama vile TB ili kukabiliana na usugu wa dawa za sasa.

Tayari WHO imebaini makundi 12 ya vijidudu vipya ambavyo havitibiki kwa dawa za sasa ikitaja magonjwa kama vile maambukizi ya njia ya mkojo na vichomi.

Kwa mujibu wa WHO hivi sasa kuna makundi  51 ya viua vijasumu vinavyofanyiwa majaribio ambapo makundi 8 tu ni mapya ilihali mengine ni dawa zilizoboreshwa.

Photo Credit
Msaidizi wa maabara anapima damu na kuandika matokeo. Picha: WHO/C. Tephava