Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wailaani Korea Kaskazini kwa kurusha kombora

UM wailaani Korea Kaskazini kwa kurusha kombora

Pakua

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa   limelaani vikali tukio la Jamhuri ya kidemkrasia ya watu wa Korea, DPRK kurusha kombora na kuvuka kisiwa cha Japan.

Kupitia taarifa iliyosomwa na rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Agosti Balozi Amr Aboulatta mwishoni mwa kikao cha dharura kilichoitishwa Jumanne jioni, wajumbe wa baraza wamesema kitendo hicho cha makusudi kinahatarisha usalama wa kikanda na wa kimataifa.

Naye mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley amesema kuwa wajumbe 15 wa baraza hilo wamezungumza kwa pamoja na kuitaka  DPRK au Korea ya Kaskazini iache mara moja mikakati ya silaha za nyuklia.

Amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusu uovu wa Korea Kaskazini na kwamba ni wakati wa utawala wa Korea Kaskazini kutambua hatari wanayojiweka.

Naye mwakilishi wa kudumu wa Japan Balozi Koro Bessho ameunga mkono taarifa hiyo ya rais wa Baraza akisema inaonyesha umoja wa chombo hicho na inatuma ujumbe thabiti kwa Korea Kaskazini kuwa jumuiya ya kimataifa haitakubali tabia ovu ya nchi hiyo.

Balozi Bessho ameisihi Korea Kaskazini iitikie wito wa kuachana an silaha hizo.

Photo Credit
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili DPRK. Picha: UM/Evan Schneider