Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yalaani ofisi zake kuingiliwa na askari wa DRC bila ruhusa

MONUSCO yalaani ofisi zake kuingiliwa na askari wa DRC bila ruhusa

Pakua

Mwakililishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo, DRC  Maman Sidikou amelaani vikali kitendo cha vikosi vya jeshi la nchi hiyo kuingia bila ruhusu kwenye ofisi za ujumbe wa umoja huo huko Kananga, jimbo la Kasai Kati.

Katika tukio hilo la Jumatatu, askari wa jeshi la DRC chini ya amri ya afisa mwandamizi Jenerali Marcellin Assumani, waliingia eneo la ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO wakimfuatilia mwandishi wa habari aliyekimbilia eneo hilo kusaka hifadhi.

Bwana Sidikou ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO amesema wamelaani sana kitendo hicho kwa kuzingatia kuwa kimetekelezwa kwa armri ya afisa mwandamizi.

Amesema maeneo ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuingiliwa bila ruhusu na ni kwa mujibu wa makubaliano ya hadhi ya vikosi vya kijeshi au SOFA ambayo DRC imetia saini na Umoja wa Mataifa.

Ametoa wito kwa serikali ya DRC kuzingatia SOFA na mikataba mingine ikiwemo ule wa kimataifa unaopatia kinga maeneo ya Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika ametaka waliohusika na kitendo hicho wachukuliwe hatua ili kuhakikisha hakirudiwi tena huku akirejelea msingi wa kisa hicho akisema kuwa masuala ya uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa demokrasia.

Photo Credit
Maman Sidikou, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na mkuu wa MONUSCO.Picha:UM/Mark Garten